Jumanne 20 Januari 2026 - 20:30
Nchi za Magharibi zinataka, ima ujisalimishe kama ng’ombe akamuliwaye na utegemee kila kitu, au uangamizwe kabisa

Hawza/ Ayatollah A’raafi, akitoa pongezi kwa uwepo wa kishujaa wa wananchi na ulinzi thabiti wa vikosi vya polisi, ujasusi na usalama, alisema: Wananchi waliingia uwanjani kwa kujitolea muhanga, na vikosi vya polisi na usalama vikailinda nchi kwa nguvu zao zote.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza A’raafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, katika kikao chake na Kamanda pamoja na Manaibu wa Uongozi wa Polisi wa Mkoa wa Qom na kundi la majeruhi wa matukio ya hivi karibuni, kilichofanyika leo katika ofisi ya Usimamizi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu, alitoa pongezi kutokana na juhudi za Jeshi la Polisi na akatoa pongezi za mwezi wa Shaaban na sherehe za Mahdawi.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu aliongeza kuwa: Kwa niaba yangu kama mwanafunzi wa dini na pia kwa niaba ya Hawza ya Kiislamu, nawapongeza nyote kwa dhati, na mashahidi watukufu wa usalama — hasa mashahidi wawili wa thamani wa matukio ya hivi karibuni ya Qom — nawaombea daraja za juu, msamaha na rehema pana za Mwenyezi Mungu.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu ya Kiislamu, akiwataja majeruhi waliokuwapo katika kikao hicho, alisema: Kwa wapendwa walioumia katika matukio haya na kufikia ukingoni mwa shahada, ninawaombea afya njema, heshima na mafanikio ya kudumu. Sisi sote kwa unyenyekevu tunawashukuru kwa kujitolea kwenu. Juhudi na mapambano ya kishujaa ya wote yanapaswa kuthaminiwa, na tunatumai mtapata thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mkurugenzi wa hawza, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali, alisema: Katika siku zilizopita niliona ni wajibu wangu kuufikia Uongozi wa Polisi wa mkoa, na kwa sababu hiyo nikakutana na kamanda mheshimiwa na baadhi ya manaibu wake ili kutoa heshima na shukrani zangu.

Kutofautisha kati ya “Maandamano na Madai ya Kisheria” na “Uharibifu na Uvunjaji wa Sheria”

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu, huku akisema kuwa maandamano ya wananchi yanaheshimiwa muda wa kuwa hayavunji mipaka ya kisheria, alieleza: Hoja muhimu ni kwamba katika nchi ambayo ina uchaguzi na demokrasia ya wananchi, na watu wanashiriki katika kuamua mustakabali wao kupitia Bunge, mabaraza ya mitaa na urais, hakuna tena uhalali wowote wa kuingia kwenye mapambano ya uharibifu na uhalifu.

Uhalali wa Jeshi la Polisi katika Kulinda Mfumo wa Kidemokrasia wa Wananchi

Mjumbe wa wanazuoni wa Baraza la Walinzi, akilinganisha hali ya Iran na baadhi ya nchi za eneo zisizo na taasisi za uchaguzi, alisema: Ni katika nchi hizo ndipo baadhi ya watu husema hakuna njia isipokuwa uharibifu. Lakini katika mfumo wenye demokrasia na uchaguzi, jeshi la polisi na walinzi wa usalama ni nguzo za kulinda demokrasia hiyo. Uhalali huu ni falsafa inayokubalika duniani kote.

Ushiriki wa Wananchi Kupitia Njia tofauti na Uchaguzi

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu alisema: Katika nchi yetu, mbali na uchaguzi, kuna ushiriki wa wananchi unaofanana na kura ya maoni ya kitaifa. Ushiriki huu ni nguzo ya wananchi katika mifumo isiyo ya uchaguzi, kama ilivyodhihirika katika hamasa ya tarehe 22 Dey.

Akirejelea maandamano ya hiari ya tarehe 22 Dey, aliongeza: Sisi wenyewe tulipokuwapo ndani ya umati kwa takriban masaa mawili, tuliona watu wa matabaka yote wakija kutoka pande zote na kusimama dhidi ya uharibifu na uvunjaji wa sheria. Huu pia ni msingi muhimu unaothibitisha Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatollah A’raafi alitaja Uislamu kuwa nguzo ya tatu, akisema: Leo dunia nzima inataka kuivunja ngome imara ya Uislamu, yaani hali ya kiroho na maadili ya kimungu ambayo leo Iran pekee ndiyo mbeba bendera wake. Nguzo hizi tatu zenye nguvu zinahalalisha kazi yenu ya kulinda nchi na kukabiliana na wavunjaji wa usalama na heshima ya maadili ya Kiislamu, kidini na kitaifa.

Kuthamini Jeshi la Polisi na Basij kama Alama za Usalama

Aliendelea kwa kutoa pongezi kwa Jeshi la Polisi na Basij, akisema: Ninasisitiza kwamba Jeshi la Polisi, kama nembo ya usalama kamili na wa kina, pamoja na Basij na taasisi nyingine, linaegemea hoja halali inayokubalika duniani na yenye mantiki ya dini. Msingi huu wa kitaifa, wa wananchi, wa kidini na wa kimapinduzi unazipa thamani kazi zote; unalindwa kimataifa na pia ni jihadi kubwa katika mantiki ya Uislamu.

Mpango wa Karne Moja wa Magharibi kwa Ulimwengu wa Kiislamu: “Kujisalimisha Kamili” au “Ardhi Iliyoteketezwa”

Ayatollah A’raafi, akizungumzia hali ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu, alifananisha kushiriki katika harakati za wananchi na uwepo ndani ya Ashura, na akaeleza: Leo Magharibi inataka kutoka kwenye nchi za Kiislamu mambo mawili: ima “kujisalimisha kikamilifu” au kugeuzwa kuwa “ardhi iliyoteketezwa.” Wakati mwingine mambo haya mawili hutekelezwa pamoja.

Alitaja janga la Syria na mauaji ya hivi karibuni huko Ghaza kama mifano ya hali hiyo, akisema: Kinachotokea Syria na uhalifu wa utawala wa Kizayuni ambao katika mwaka mmoja uliopita umetekeleza mauwaju ya watu elfu sabini, ni uthibitisho wa mtazamo huu. Asipoelewa uchambuzi huu, mtu anaweza kufafanua matatizo makuu kwa hoja nyepesi kama matatizo ya kiuchumi.

Tahadhari Kuhusu Chaguo la “Kuwa Ng’ombe wa Kukamuliwa” au “Kufutwa Kabisa”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alisema: Suala kuu ni kwamba Magharibi inataka ulimwengu wa Kiislamu ima ujisalimishe kama “ng’ombe wa kukamuliwa” na utegemee kila kitu, au uangamizwe kabisa. Huu ni mpango wa karne moja wa Magharibi ambao leo unatekelezwa kwa nguvu zaidi, nchi baada ya nchi.

Ayatollah A’raafi alirejelea hali ya baadhi ya nchi za eneo hilo, akisema: Hata zile zenye ustawi wa juu wa juu juu, nguzo zao zote zinategemea wengine. Unawezaje kuzungumzia ulinzi wa kujitegemea Saudi Arabia au Falme za Kiarabu? Silaha na mifumo yao yote iko mikononi mwa Israel na Marekani. Hata wakipewa nguvu kiasi gani, kwa kuwa uongozi hauko mikononi mwao, hauna thamani ya kweli. Aliongeza kuwa: Matakwa ya Magharibi ni utiifu kamili, na kama hayakubaliwi, lengo ni kuunda “ardhi iliyoteketezwa isiyo na ulinzi.”

Kulinda Nchi ni Jihadi Halali Dhidi ya Matakwa ya Adui

Ayatollah A’raafi alisisitiza kuwa; kulinda nchi ni jihadi halali, akasema: Katika mantiki ya kimataifa na ya Kiislamu, ulinzi wa nchi na rasilimali zake una hadhi kubwa.

Kufananisha Msimamo wa Adui na Kipindi cha Ashura

Alisema: Matakwa ya adui leo kwenye ulimwengu wa Kiislamu ni yale yale ambayo Imam Hussein (a.s.) aliyakataa kwa kauli yake: (Udhalili upo mbali nasi).

Trump: Mharakishaji wa Sera za Kibeberu

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu alisema: Trump, kwa ujinga wake, anaharakisha mchakato huu, la sivyo matakwa haya ya adui yalikuwapo hata kabla ya Mapinduzi.

Hali ya Sasa: Uchaguzi kati ya Kujisalimisha, Kuangamizwa au Jihadi

Mjumbe wa Baraza la Waangalizi alisema: Tuko katika hali ambayo ili kutoka kwenye dimbwi hili bila kujisalimisha wala kuangamia, njia pekee ni jihadi. Jihadi hii ina uhalali wa kimataifa na pia ni jihadi sahihi ya Kiislamu, leo hatuna njia nyingine.

Jihadi Chini ya Uongozi wa Wilaya Hutoa Maana ya Mapambano

Aliongeza kuwa: Thamani ya juhudi hizi iko katika kusonga mbele chini ya uongozi wa Wilaya. Jihadi bila uongozi wa haki ni kujiua, lakini chini ya uongozi sahihi, kila kitu hupata maana na jihadi hutimia.

Umuhimu wa Kuwa Macho katika Nyakati Nyeti za Taifa

Ayatollah A’raafi, akirejelea matukio ya kihistoria kama mapinduzi ya tarehe 28 Mordad 1953 HS, alisema: Siku moja tu ya uzembe na kushindwa kwa vikosi vya kijeshi kudhibiti hali ilisababisha miaka 25 ya utegemezi na dhulma. Wengi walikaa kimya, na wahuni kadhaa wakatawala. Aliongeza kuwa katika matukio ya hivi karibuni pia kulikuwa na juhudi za maadui kutumia madai halali ya wananchi vibaya.

Pongezi kwa Ushirikiano wa Wananchi na Vikosi vya Usalama

Mjumbe wa Baraza la Walinzi alisema: Wananchi walijitokeza kwa kujitolea, na vikosi vya usalama vililinda nchi kwa nguvu zao zote. Ushirikiano huu uliweza kudhibiti hali ngumu kuliko vita vya miaka minane.

Kusimama kwa Jeshi la Polisi katika “Wakati wa Hatima”

Alisema: Leo mmekuwapo katika kona muhimu ya historia na mkazuia adui kufanikiwa dhidi ya uhuru na heshima ya Iran na Uislamu.

Kuthamini Juhudi katika Wakati wa Kihistoria

Ayatollah A’raafi alisema: Huu ulikuwa wakati wa hatima ya Uislamu, Ushia, Mapinduzi ya Iran na uhuru wa taifa. Ninyi kwa kushirikiana na wananchi mlitengeneza tukio kubwa.

Kufananisha na “Pigo la Imam Ali (a.s.) Siku ya Khandaq”

Alisema: Pigo la Imam Ali (a.s.) siku ya Khandaq lilikuwa ibada bora zaidi kwa sababu lilitolewa kwa ikhlasi na katika wakati ambao kama lisingetolewa, kila kitu kingeanguka, ninyi pia mlijitolea katika wakati wa kipekee.

Pongezi za Mwisho kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi la Taifa

Mwishoni, Ayatollah A’raafi aliwakilisha shukrani maalumu za Hawza kwa Jenerali Radan, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Taifa, na kwa wafanyakazi wote wa FARJA, akisema: Mwenyezi Mungu ayakubali mapambano haya na atufanye sisi sote kuwa askari wa Uislamu, wa Imam Mahdi (a.j.), wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa Kiongozi Mkuu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha